YANGA YAHAMISHIA ZANZIBAR MECHI ZAKE ZA KUNDI B LIGI YA MABINGWA AFRIKA

KLABU ya Yanga imesema kwamba itatumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwa mechi zake zote za Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Ally Shaaban Kamwe amesema kwamba hatua hiyo inafuatia tathimini iliyofanywa na uongozi wa kwa maslahi mapana ya klabu.
“Baada ya uongozi kufanya Tathimini na kuangalia maslahi mapana ya Klabu yetu, nipende kuwatangazia kuwa mechi zetu zote tatu za nyumbani kwenye hatua ya Makundi, tutatumia uUwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar,” amesema Kame na kuongeza;
“Niwaombe sana mashabiki na Wanachama wetu kutoka visiwa vya Pemba na Unguja kujiandaa kuipokea timu na maandalizi ya nguvu kuelekea mchezo wa kwanza wa nyumbani dhidi ya FAR RABAT. Wanachama wengine kutoka mikoani tujiandae pia, tupo kwenye kundi gumu lakini tukiwa wamoja, tukiendelea kushiriana kwa umoja wetu tutatoboa, ”.

Yanga SC imepangwa Kundi B katika Hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wapinzani wote watatu kutoka nchi Kaskazini mwa Afrika.
Wapinzani hao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri, AS FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria.
Timu nyingine ya Tanzania, Simba SC imepangwa Kundi D pamoja na Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia, Petro de Luanda ya Angola na Stade Malien ya Mali.
Kundi A liwakautanisha mabingwa watetezi, Pyramids FC ya Misri, mabingwa wa Kimbe la Shirikisho Afrika, RS Berkane ya Morocco, Rivers United ya Nigeria na Power Dynamos ya Zambia.
Kundi C linaundwa na mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Al Hilal ya Sudan, MC Alger ya Algeria na St Éloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Yanga wataanzia nyumbani dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco Novemba 22, kabla ya kusafiri kwenda Algeria kumenyana JS Kabylie Uwanja wa Hocine Aït Ahmed mjini Tizi Ouzou kati ya Novemba na 28 na 29 na kwenda Misri kukamilisha mzunguko wa kwanza kwa kumenyana na Al Ahly Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo kati ya Januari 23 na 24 mwakani, 2026.
Mzunguko wa pili, Yanga wataanzia nyumbani tena dhidi ya Al Ahly kati ya Januari 30 na 31, kabla ya kusafiri kwenda Morocco kumenyana na AS FAR Rabat kati ya Februari 6 na 7 Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Jijini Rabat – na kurejea nyumbani kukamilisha mechi zake za Kundi B kwa kumenyana na JS Kabylie kati ya Februari 13 na 14.




