YANGA SC YATOKA SULUHU NA TRA UNITED MECHI YA KIRAFIKI GHYMKANA

KLABU ya Yanga imetoa sare ya bila mabao na TRA United, zamani Tabora United katika mchezo wa kirafiki mapema leo Uwanja wa Ghymkana, Dar es Salaam.
Inakuwa sare ya pili mfululizo kwa Kocha Mfaransa, Romain Folz kufuatia nyingine ya 0-0 katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mbeya City Septemba 29 Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya baada ya mwanzo mzuri wa ushindi mfululizo ikiwemo kutwaa ya Ngao ya Jamii.
Matokeo ya leo yanaongeza presha kwa uongozi kuachana na Kocha huyo kijana wa umri wa miaka 35 ambaye tayari kwa kiais kikubwa mashabiki hawajaridhishwa naye hata wakati timu inashinda.

Yanga inajiandaa na mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Silver Strikers Oktoba 18 Uwanja wa Taifa wa Bingu, Lilongwe nchini Malawi, kabla ya timu hizo kurudiana Oktoba 25 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.



