WYDAD ATHLETIC YAMTAMBULISHA RASMI AZIZ KI
KLABU ya Wydad Athletic imemtambulisha rasmi kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki kuwa mchezaji mpya baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Yanga ya Tanzania.
Utambulisho huo umefanyika usiku wa kuamkia leo – saa chache tu baada ya Yanga kumuaga Aziz Ki kufuatia kuwa naye kwa misimu mitatu tangu awasili kutoka ASEC Mimosas.
Wydad Athletic ya Morocco na usajili wake umeharakishwa ili akacheze michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA inayotarajiwa kuanza Juni 14 hadi Julai 13 nchini Marekani ikishirikisha timu 32 kutoka Mabara sita – nne kutoka Afrika, nyingine ni Al Ahly ya Misri, Espérance ya Tunisia na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.
Wydad imepangwa Kundi G pamoja na Manchester City ya England, Al Ain ya Falme za Kiarabu (UAE) na Juventus ya Italia, wakati Al Ahly ipo Kundi A pamoja na Palmeiras ya Brazil, FC Porto ya Ureno na Inter Miami CF ya Marekani.
Mamelodi Sundowns Kundi F pamoja na Fluminense ya Brazil, Borussia Dortmund ya Ujerumani na Ulsan HD ya Korea Kusini na Espérance Kundi D pamoja na Flamengo ya Brazil, Chelsea ya England na mshindi wa mechi ya mchujo kati ya Los Angeles FC ya Marekani na América ya Mexico.
Aziz alijiunga na Yanga Julai mwaka 2022 akitokea ASEC Mimosas ambayo aliichezea kuanzia Januari mwaka 2021 alipowasili akitokea AFAD Djékanou ya Ivory Coast pia.
Kisoka Azi Ki alianzia timu za vijana za Hispania, Rayo U19 mwaka 2015 na San Roque Lepe mwaka 2016, kabla ya kwenda Cyprus ambako alichezea Omonia Nicosia kuanzia 2016 hadi 2017, ingawa katikati alipelekwa kwa mkopo Aris Limassol ya huko pia.
Mwaka 2018 alijiunga na Nea Salamis ya Cyprus pia hadi 2019 aliporudi Ivory Coast na kuchezea AFAD Djékanou na ASEC kabla ya kuja Tanzania kujiunga na Yanga.
Katika misimu yake mitatu ya kuwa Yanga amecheza jumla ya mechi rasmi 114 na kufunga mabao 57 na pasi za mabao 32, akishinda jumla ya mafaji nane, Ligi Kuu, Kombe la TFF na Ngao ya Jamii yote mara mbili pamoja na Kombe la Muungano na Kombe la Toyota.
Msimu uliopita, 2023-2024 ulikuwa wa mafanikio zaidi kwake akitwaa Tuzo za Mfungaji Bora, Mchezaji Bora na Kiungo Bora wa Ligi Kuu pamoja na kuiongoza Yanga kuwafunga watani, Simba SC 5-1.
Zaidi ya mafanikio ya ndani ya Uwanja, Aziz Ki pia amepata mke Tanzania, amemuoa Mwanamitindo Hamisa Mobetto na hivi sasa tayari yupo naye Ivory Coast.




