TWIGA STARS YAANZA VIBAYA WAFCON, YACHAPWA 1-0 NA MALI

TANZANIA imeanza vibaya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuchapwa bao 1-0 na Mali katika mchezo wa Kundi C usiku huu Uwanja wa Manispaa ya Berkane Jijini Berkane nchini Morocco.
Bao pekee la Les Aiglonnes (Tai wa kike) lililoizamisha Twiga Stars limefungwa na kiungo wa Fatih Karagümrük ya Uturuki, Saratou Traoré dakika ya 45.
Mchezo uliotangulia wa Kundi C, Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ iliichapa Ghana ‘Black Queens’ 2–0 Uwanja wa Honneur mjini Oujda.

Mabao ya Mabinti wa Kisauzi yaliyowaduwaza Malkia Weusi yamefungwa na winga wa Glasgow City ya Scotland, Linda Maserame Motlhalo dakika ya 28 kwa penalti na mshambuliaji wa Liga MX Femenil ya Mexico, Jermaine Seoposenwe dakika ya 33.
Mechi zijazo za Kundi C, Tanzania itacheza na Afrika Kusini Uwanja wa Honneur, Oujda na Mali itaumana Ghana Uwanja wa Berkane Julai 11.





