SENEGAL YAICHAPA ENGLAND 3-1 NA KUWEKA REKODI MPYA AFRIKA

WACHEZAJI wa England walizomewa jana baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Senegal katika mechi ya kirafiki Uwanja wa City Ground, West Bridgford, Nottinghamshire, England.
Ushindi huo unamaanisha Senegal inaweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kupata ushindi dhidi ya England katika mchezo wowote kihistoria.
Ilikuwa ni mechi ambayo mbinu za Kocha Mjerumani wa Three Lions Thomas Tuchel zilifeli kabisa licha ya kuanza vyema na kupata bao la mapema lililofungwa na mshambuliaji wa mabingwa wa Ujerumani, Harry Edward Kane wa Bayern Munich dakika ya saba.
Mabao ya Simba wa Teranga yote yalifungwa na washambuliaji wa pembeni, Ismaïla Sarr wa Watford ya England dakika ya 40 na nyota wanaocheza Ufaransa, Mouhamadou Habib Diarra wa Strasbourg dakika ya 62 na Cheikh Tidiane Sabaly wa Metz dakika ya 90’+3.
Kane ndiye mchezaji pekee aliyekuwemo kwenye kikosi cha kilichoanza jana cha Three Lions kutoka kile kilichoshinda 1-0 dhidi ya Andorra wiki iliyopita, jambo ambalo lilimfanya Kocha Tuchel ajilaumu kwa mabadiliko aliyoyafanya.




