RASMI KAIZER CHIEFS IMEACHANA NA NABI, KAZE KUIONGOZA TIMU KUMALIZIA MSIMU

KLABU ya Kaizer Chiefs FC imethibitisha kuachana na Kocha wake Mkuu, Mtunisia Nasreddine Nabi baada ya makubaliano ya pande zote mbili.
Katika taarifa yake, Kaizer Chiefs FC imemshukuru Kocha Nabi kwa mchango wake katika kipindi chake akiwa na klabu hiyo na inamtakia kila la kheri anakoelekea.
Kwa upande wake, Kocha Nabi ametoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa Kaizer Chiefs FC, wafanyakazi, wachezaji na mashabiki kwa sapoti yao wakati wote akiwa kwenye klabu hiyo.
Kwa sasa Kaizer Chiefs FC itakuwa chini ya waliokuwa Wasaidizi wa Nabi, Mtunisia Khalil Ben Youssef na Mrundi Cedric Kaze ambao wataiongoza timu kwa muda uliosalia wa msimu wa 2025/26.

Nabi amekuwa nje ya kikosi tangu mwanzoni mwa Septemba katika mwanzo wa msimu wake wa pili na Amakhosi baada ya msimu wake wa kwanza kuwasaidia Glamour Boys kumaliza ukame wa mataji wa muongo mmoja kwa kushinda Kombe la Nedbank, ingawa kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini ‘PSL’ walimaliza nafasi ya tisa.
Dalili mbaya za Nabi na Kaizer katika msimu wake wa pili zilianza mapema tu mwanzoni mwa msimu wa 2025/26 alikuwa Tunisia akishughulikia masuala ya kifamilia huku ‘Machifu’ wakianza vyema kampeni.





