PACOME ATOKEA BECHI IVORY COAST YAICHAPA KENYA 3-0 NA KUFUZU KOMBE LA DUNIA

KIUNGO wa Yanga SC ya Tanzania, Peodoh Pacome Zouzoua jana alitokea benchi kipindi cha pili timu yake, Ivory Coast ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kenya katika mchezo wa mwisho wa Kundi F Kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 uliofanyika Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara Jijini Abidjan.
Ivory Coast imeungana na washindi wengine was aba wa makundi, Misri (A), Senegal (B), Afrika Kusini (C), Cape Verde (D), Morocco (E), Algeria (D), Tunisia (H) na Ghana (I) kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
Pacome aliingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Nicolas Pépé wa Villarreal ya Hispania – wakati huo tayari Tembo wanaongoza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na mshambuliaji wa Al-Ahli ya Saudi Arabia, Franck Yannick Kessié dakika ya saba na winga Yan Diomande wa RB Leipzig ya Ujerumani dakika ya 54.
Kulikuwa kuna wachezaji wawili wa Yanga uwanjani jana – mwingine ni kiungo Duke Abuya aliyeingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa Al-Arabi ya Qatar, Michael Olunga.
Pacome akiwa uwanjani, Ivory Coast ikapata bao la tatu lililofungwa na winga wa Manchester United, Amad Diallo dakika ya 84 na kujihakikishia uongozi wa Kundi F na tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia za mwakani zinazoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Mexico na Canada.
Ikumbukwe mechi iliyopita Pacome alicheza kwa dakika zote 90 Tembo wa Ivory Coast wakiibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya wenyeji, Shelisheli Uwanja wa Côte d’Or National Sports Complex Jijini Saint Pierre nchini Mauritius.
Siku hiyo mabao ya Tembo yalifungwa na Ibrahim Sangaré dakika ya saba kwa penalti, Badobre Agbadou dakika ya 17, Oumar Diakité dakika ya 32, Evann Ludovic Guessand dakika ya 39 na Yan Diomande Diomande dakika ya 55, Simon Adingra dakika ya 67 na Franck Kessié dakika ya 90.

Ivory Coast imemaliza na pointi 26,moja zaidi ya Gabon iliyomaliza nafasi ya pili, ambayo inaungana na Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Cameroon kwenda kuwania nafasi ya Kufuzu Kombe la Dunia kupitia Mechi za Mchujo.
Katika Mechi za Mchujo wa Afrika ziakazofanyika nchini Morocco – kwenye Nusu Fainali Nigeria itamenyana na Gabon na Cameroon dhidi ya DRC Novemba 13 na fainali itafutaia Novemba 16 na mshindi atakwenda kwenye Mchujo wa mwisho wa Mabara yote utakaofanyika Machi mwakani nchini Mexico ukishirikisha jumla ya timu sita.
Washiriki wengine ni Bolivia iliyomaliza nafasi ya saba Amerika Kusini (CONMEBOL), New Macedonia ambayo ni mshindi wa Pili wa Raundi ya Tatu Bara la,Oceania (OFC), mshindi wa Mchujo wa Raundi ya Tano Bara la Asia (AFC) ambaye atapatikana Novemba 18, mshindi wa pili Bora wa Raundi ya Tatu Amerika ya Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) ambaye atapatikana mwezi Novemba pia.



