NGOMA AAGA SIMBA SC NA KUWAACHIA USIA; “ MKIWA NA FADLU MAZURI YANAKUJA”

KIUNGO wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fabrice Luamba Ngoma (31) ameaga katika klabu ya Simba baada ya misimu miwili ya kuwa na Wekundu hao wa Msimbazi akishinda taji moja na kuifikisha timu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ngoma ameandika kwenye kurasa za mitandao ya kijamii akiaga na kuwashukuru viongozi waliofanikisha usajili wake Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya klabu, Mohamed Gulam Dewji na Mjumbe, Salum Abdallah Muhene huku akijivunia mafanikio machache aliyovuna na Wekundu hao wa Msimbazi.
“Habari za asubuhi wote. Nilitaka kuchukua muda huu kuwashukuru wote walionifanya nijisikie nyumbani hapa Simba. Asante kwa Mr Salum Try Aagain na Boss MO walionileta hapa misimu miwili iliyopita,” ameandika mapema leo kwenye ukurasa wake wa Instgram.
“Asante kwa kocha, wafanyikazi, wachezaji ambao tulishirikiana pamoja chumba cha kubadilishia nguo.
Hatukuweza kufikia baadhi ya malengo yetu, lakini kumbukumbu zote zitabaki milele katika akili na moyo wangu.
Kwenu mashabiki wa Simba asanteni kwa sapoti yenu. Msiiangushe klabu kabisa, nyakati bora zaidi ziko mbele hususan ukiwa na kocha kama Fadlu,”.

Ngoma aliwasili Simba SC Julai 14, mwaka 2013 akitokea Al-Hilal Omdurman ya Sudan katika misimu hiyo miwili ameshinda taji moja tu na Simba, Kombe la Muungano mwaka jana, 2024 – lakini kitu kikubwa zaidi ni Medali ya Fedha ya Kombe la Shirikisho mwaka huu.
Ngoma aliibukia klabu ya MK Etanchéité ya kwao, Kinshasa mwaka 2017 alikocheza kwa miezi kadhaa kabla ya kuhamia Ifeanyi Ubah ya Nigeria alikocheza hadi 2019 akareejea nyumbani kujiunga na AS Vita mwaka 2019.
Mwaka 2022 alijiunga na Raja Casablanca ya Morocco alikocheza hadi 2023 akahamia Al-Fahaheel ya Kuwaiti alikocheza kwa nusu msimu kabla ya kwenda Al-Hilal Omdurman.





