MKONGO BOLA JEPHTE KITAMBALA AJIUNGA NA AZAM FC

KLABU ya Azam FC imekamilisha usajili wa mshambuliaji Bola Jephte Kitambala (26) kutoka AS Maniema Union ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Azam FC imemtambulisha mchezaji huyo akiwa anasaini mkataba na kukabidhiwa jezi na Mkurugenzi wa Fedha wa klabu hiyo, Abdulkarim Shermohamed ‘Karim Mapesa’.
Bola Jephte Kitambala aliibukia kwenye timu ya vijana ya TP Mazembe ya kwao, DRC kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa mwaka 2019 ambako mwaka 2020 alipelekwa kwa mkopo CS Don Bosco.
Mwaka 2021 alirejea Mazembe akatolewa tena kwa mkopo AS Maniema Union mwaka 2023 kabla ya kumaliza mkataba mwaka jana na kujiunga moja kwa moja timu hiyo ambayo ameichezea hadi sasa anahamia Azam FC.


Kitambala anakuwa mchezaji mpya wa sita Azam FC baada ya kipa Aishi Manula kutoka Simba SC, beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union na nyota wawili waliokuwa wanacheza Ligi Kuu ya Misri, kiungo Himid Mao Mkami kutoka Ghazl El Mahalla na mshambuliaji Muhsin Makame kutoka Zed FC, wakati mchezaji mwingine mpya ni kiungo mshambuliaji Pape Doudou Diallo kutoka Generation Foot ya kwao, Senegal.
Azam FC pia imempandisha Nahodha wa timu yake ya vijana, beki wa kati Ally Hassan Chamulungu.
Kwa sasa kikosi cha Azam FC kimeweka kambi Karatu, Arusha chini ya Kocha Mkuu, Mkongo pia Jean-Florent Ibenge na wiki ijayo inatarajiwa kwenda kwa maandalizi zaidi.
Azam FC inatarajiwa kuuanza msimu kwa kumenyana na Yanga SC katika Nusu Fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii Septemba 11 na mshindi atakutana na mshindi kati ya Simba SC na Singida Black Stars katika Fainali Septemba 14.
Baada ya hapo wataingia kwenye mchezo wa Raundi ya kwanza ya mchujo wa kuwania kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya El Merreikh Bantiu ya Sudan Kusini.
Aidha, Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, 2025/2026 inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu 2025 – wastani wa wiki mbili tu baada ya kumalizika kwa na Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).
Msimu mpya wa Ligi Kuu umelazimika kuchelewa kutokana na Tanzania mwenyeji mwenza wa CHAN pamoja na jirani zake, Kenya na Uganda zinazotarajiwa kuanza Agosti 2 hadi 30, mwaka huu.




