MAURITANIA YATANGULIZA MGUU MMOJA ROBO FAINALI CHAN

TIMU ya taifa ya Mauritania ‘Simba wa Chinguetti’ usiku wa jana iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Burkina Faso ‘The Stallions’ katika mchezo wa Kundi B Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee la mshambuliaji wa klabu ya
ASAC Concorde Nouakchott, Alassane Diop dakika ya 45’+9 na kwa ushindi huo, Mauritania wanafikisha pointi saba baada ya kucheza mechi zao zote nne za Kundi B.
Mechi nyingine ya Kundi B mapema jana Madagascar iliichapa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) 2-0 hapo hapo Uwanja wa Mkapa mabao ya winga Toky Niaina Rakotondraibe dakika ya 84 na kiungo Lalaina Cliver Rafanomezantsoa dakika ya 90’+4.
Mauritania sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya Tanzania ambayo imekwishafuzu Robo Fainali kwa pointi zake tisa za mechi tatu – wakiwa mbele ya Madagascar yenye pointi nne, Burkina Faso pointi tatu, wakati Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) inashika mkia baada ya kufungwa mechi zote tatu za awali.
Mauritania sasa itaiombea Burkina Faso iifunge Madagascar Jumamosi katika mchezo wa mwisho au timu zitoke sare ndio ifuzu Robo Fainali.
Kama Madagascar itashinda basi itamaliza na pointi saba sawa Mauritania na timu ya kuungana na Tanzania kwenda Robo Fainali kutoka Kundi B itatapatikana kwa mujibu wa kanuni – kama wastani wa mabao na matokeo ya mechi baina yao.




