KARIA NA HERSI WATEULIWA KAMATI TOFAUTI ZA MASHINDANO FIFA

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Soka ya Ufukweni ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Naye Rais wa klabu ya Yanga SC na Mwenyekiti wa Chama cha Klabu Afrika (ACA), Hersi Ally Said ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano Klabu ya Wanaume ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kwa mujibu wa barua ya FIFA kwenda kwa Hersi, uteuzi wake utadumu kwa miaka minne kuanzia mwaka huu 2025 hadi mwaka 2029.
Rais huyo wa Yanga anakuwa Mtanzania pekee na kwa ujumla mtu kutoka Afrika Mashariki na Kati kwenye Kamati hiyo na wa kwanza kwa ujumla kuwahi kuteuliwa kwenye Kamati hiyo ya FIFA.
Viongozi mbalimbali wa Afrika wameteuliwa kwenye Kamati tofauti za FIFA, Mtanzania mwingine, Neema Haji akiteuliwa kwenye Kamati ya Vijana ya Mashindano ya Wasichana ya CAF.
Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kamati ya Sheria za Mchezo ya FIFA.





