FOUNTAIN GATE YAICHAPA STAND UNITED 3-1 SHINYANGA

TIMU ya Fountain Gate imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kubaki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji, Stand United jioni ya leo Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.
Katika mchezo huo wa kwanza wa mchujo wa Ligi Kuu na Championship mabao ya Fountain Gate yamefungwa na Kassim Haruna ‘Tiote’ dakika ya 28, Sadik Said Ramadhan ‘Immobile’ dakika ya 65 na Mudrik Sheikh Gonda dakika ya 85, wakati la Stand United alijifunga beki Joram Mgeveke dakika ya 44.
Timu hizo zitarudiana Jumanne ya Julai 8 na mshindi wa jumla atakamilisha idadi ya timu 16 za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu ujao.
Ikumbukwe Fountain Gate wameporomoka kwenye mchujo wa Ligi Kuu baada ya kutolewa na Tanzania Prisons, wakati Stand United walifuzu mchujo wa Championship baada ya kuitoa Geita Gold.




