CAF YAHALALISHA USHIRIKI WA TAIFA STARS AFCON DESEMBA MOROCCO

KAMATI ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeitupilia mbali Rufaa ya Shirikisho la Soka Guinea (GFF) dhidi ya Tanzania juu ya mchezo wa mwisho wa Kundi H kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Morocco.
Tanzania iliifunga Guinea 1-0 Novemba 19, mwaka 2024 bao la mshambuliaji wa Al Talaba ya Iraq, Simon Happygod Msuva dakika ya 61 akimalizia pasi nzuri ya kiungo wa Yanga ya nyumbani, Dar es Salaam, Mudathir Yahya Abbas Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mchezo huo, Guinea iliyoongozwa na mshambuliaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Serhou Yadaly Guirassy ilimkatia rufaa beki Ibrahim Mohamed Ame kwamba hakuwa raia wa Tanzania.
Hata hivyo, baada ya kuthibitishiwa uraia wake kufuatia malalamiko yao ya awali Kamati ya Nidhamu ya CAF — wakabadilisha madai yao na kukata Rufaa Kamati ya Rufaa ya Bodi hiyo ya soka Afrika wakisema alivaa jezi tofauti na iliyoandikwa kwenye orodha ya wachezaji, hivyo iliwavuruga na kusababisha wapoteze mechi hiyo.

Lakini huko nako wamekwama na sasa Tanzania inaendelea na maandalizi ya AFCON itakayofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani, 2026.
Taifa Stars ilimaliza na pointi 10, nyuma ya vinara Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyomaliza na pointi 12 na zote zikafuzu AFCON 2025, huku Guinea iliyomaliza na pointi tisa ikimaliza nafasi ya tatu, mbele ya Ethiopia iliyovuna pointi nne.
Taifa Stars wamefuzu AFCON kwa mara ya nne kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 Misri na 2023 nchini Ivory Coast na safari hii inakuwa mara ya kwanza inafuzu Fainali mbili mfululizo.
Katika AFCON ya Morocco Desemba mwaka huu, Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Nigeria, Tunisia na Uganda.
Ikumbukwe kwa tiketi ya uenyeji wakishirikiana na Kenya na Uganda – Tanzania pia watacheza Fainali za AFCON za mwaka 2027.





