TAIFA STARS YAICHAPA ESWATINI 2-1 KOMBE LA COSAFA

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Eswatini katika mchezo wa mwisho wa Kundi C Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) jioni ya leo Uwanja wa Toyota Free States Jijini Bloemfontein, Afrika Kusini.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Taifa Stars – kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya Eswatini kuanza kupata bao kupitia kwa Magagula Andy Junior dakika ya 29.
Taifa ikazinduka kabla ya mapumziko na kusawazisha bao hilo kupitia kwa winga wa Azam FC, Iddi Suleiman ‘Nado’ dakika ya 37 kabla ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Shekhan Ibrahim Khamis kufunga bao ka ushindi dakika ya 69.

Taifa Stars inamaliza na pointi tatu nafasi ya pili Kundi C nyuma ya Madagascar yenye pointi nne ambayo inakwenda Nusu Fainali, wakati Eswatini yenye pointi moja nayo inaungana na Tanzania kurejea nyumbani.
Timu nyingine zilizotinga Nusu Fainali ni Afrika Kusini (Kundi A), Angola (Kundi B) na Comoro Kundi D.
Nusu zitachezwa Ijumaa Angola na Madagascar kuanzia Saa 9:00 Alasiri na Afrika Kusini dhidi ya Comoro kuanzia Saa 12:00 jioni zote Uwanja wa Toyota Free State, Bloemfontein.
