CRISTIANO RONALDO AMALIZA UTATA, ASEMA ANABAKI AL-NASSR

MWANASOKA Bora wa zamani wa Duni, Cristiano Ronaldo ameripotiwa kumaliza kitendawili cha mustakabali wake kwa kusema ataendelea kuchezea Al-Nassr inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia ‘Saudi Pro League’ pia akidhamiria kucheza Fainali zijazo za Kombe la Dunia.
“Hakuna kitakachokwenda kubadilika. Kucheza Al-Nassr? Ndio,” alinukuliwa akisema mapema leo baada ya Nahodha huyo kuiongoza Ureno kutwaa taji la Ligi ya Mataifa Ulaya Jijini Munich nchini Ujerumani usiku wa jana.
Ronaldo (40) alijiunga na Al-Nassr mwaka 2023 baada ya kutofautiana na Kocha wa Erik ten Hag alipokuwa Manchester United kwa kusaini mkataba ambao utafikia tamati Juni 30.
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino hivi karibuni alipendekeza kwamba Ronaldo anaweza kuhamia klabu iliyofuzu Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA na mwenyewe alithibitisha kufanyika kwa mazumgumzo hayo, ingawa akasema hatakuwepo kwenye michuano hiyo itakayofanyika Marekani.
Jumapili usiku Ureno iliifunga Hispania kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2 ndani ya dakika 120 naRonaldo taji la tatu na timu yake ya taifa – mengine Kombe la Mataifa Ulaya ‘Euro’ 2016 na UEFA Nations League mwaka 2019.
“Nina mataji mengi, lakini huko hakuna kilicho bora Zaidi ya kushinda na timu ya taifa,” alisema mshindi huyo wa Tuzo tano za Ballon d’Or.
Ronaldo alifunga bao la kusawazisha katika sare ya 2-2 na Ufaransa dakika ya 61, kabla ya kupumzishwa dakika ya 88 kufuatia kuumia misuli, ingawa timu yake ilishinda kwa matuta. Pia alifunga katika ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa Nusu Fainali Jumatano dhidi ya wenyeji, Ujerumani.
Mabao hayo mawili yanamfanya Ronaldo akifikishe jumla ya manao 138 katika mechi 221 alizoichezea Ureno, ambazo zote ni rekodi za dunia katika soka ya wanaume.