LAMINE YAMAL AFUNGA MAWILI HISPANIA YAICHAPA UFARANSA YA MBAPPE 5-4

MWANASOKA nyota chipukizi wa Hispania, Lamine Yamal amefunga mabao mawili La Roja ikiibuka na ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa Nusu Fainali Ligi ya Mataifa ya Ulaya usiku huu Uwanja wa MHPArena Jijini Stuttgart nchini Ujerumani.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Refa Michael Oliver wa England – mbele ya mashabiki 51,724, Yamal alifunga mabao yake dakika ya 54 kwa penalty na 67, wakati mabao mengine yamefungwa na winga wa Athletic Bilbao, Nico Williams dakika ya 22, viungo Mikel Merino wa Arsenal na Pedro González ’Pedri’ anayecheza naye Barcelona dakika ya 55.
Mabao ya Ufaransa yamefungwa na mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe kwa penalti dakika ya 59, kiungo wa Lyon, Rayan Cherki dakika ya 79, Dani Vivian wa Athleitic Bilbao aliyejifunga dakika ya 84 na Randal Kolo Muani dakika ya 90+3′.
Kwa matokeo hayo – mabingwa wa Ulaya, Hispania wanatinga Fainali ya UEFA Nations League kwa mara ya tatu mfululizo ambako watakutana na jirani zao wa Iberia, Ureno Jumamosi kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Allianz Arena Jijini Munich.
Kwa upande wao Ufaransa watajaribu kupoza machungu mbele ya wenyeji, Ujerumani katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Jumamosi pia kuanzia Saa 9:00 Alasiri hapo hapo MHPArena.