REFA SASII AFUNGIWA MIEZI SITA, FADLU NA SOWAH WATOZWA FAINI

REFA Heri Sasii amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kuumudu mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baina ya wenyeji, Simba SC dhidi ya Singida Black Stars Mei 28 Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) jioni ya leo baada ya kikao chake cha Juni 2 kupitia matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi imesema kwamba refa Sasii alifanya matukio mengi yaliyoashiria kushindwa kutafsiri vyema sharia 17 za mchezo.
Aidha, Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadluraghman Davids raia wa Afrika Kusini naye ametozwa Faini ya Sh. Milioni 2 kwa kosa la kuishutumu Bodi kwamba ina ajenda tofauti kwa ratiba ambayo timu yake inapangiwa katika ligi hiyo.
Fadlu alitoa tuhuma hizo wakati anafanyiwa mahojiano na Azam TV baada ya mchezo huo ambao timu yake iliibuka na ushindi wa 1-0m bao pekee la mshambuliaji wa Kimataifa wa Uganda, Steven Dese Mukwala dakika ya 43 akimalizia kazi nzuri ya kiungo Muivory Coast, Jean Charles.
Nayo klabu ya Simba imetozwa Faini pia ya Sh. Milioni 5 baada ya mashabiki wake kurusha chupa za maji uwanjani wakati wa mchezo huo dhidi ya Singida Black Stars.
Naye mshambuliaji Mghana wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah amtozwa Faini ya Sh. Milioni 1 kufuatia kuwaonyesha ishara ya matusi mashabiki wa Simba pamoja na kung’oa kibendera cha kona.






