SINGIDA BLACK STARS YAICHAPA SIMBA SC 3-1 NUSU FAINALI KOMBE LA CRDB

TIMU ya Singida Black Stars imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba SC jioni ya leo Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.
Mabao yote ya Singida Black Stars yamefungwa na wachezaji kutoka Ghana, mshambuliaji Jonathan Sowah dakika ya 17 na kiungo Emmanuel Kwame Keyekeh mawili dakika ya 35 na 48, wakati bao pekee la Simba SC limefungwa na kiungo Muivory Coast, Jean Charles Ahoua dakika ya 49.
Bao la kwanza langoni alikuwa kipa Mguinea, Moussa ‘Pin Pin’ Camara, lakini akatoka nje dakika ya 25 baada ya kuumia kufuatia kugongana na Sowah – nafasi yake ikachukuliwa Ally Salim aliyeruhusu mabao mengine mawili ya Kayekeh.
Katika Fainali mwishoni mwa mwezi ujao – Singida Black Stars watakutana na Yanga SC ambayo katika Nusu Fainali iliitoa JKT Tanzania kwa kuichapa mabao 2-0 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Huu unakuwa msimu wa nne mfululizo Simba wanashindwa kufika Fainali ya michuano hiyo, mara mbili wakitolewa katika Nusu Fainali 2021-22 wakitolewa na Yanga kwa kufungwa 1-0 bao pekee la Feisal Salum dakika ya 25 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza na 2022-23 na wakitolewa na Azam FC kwa kufungwa 2-1 Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Msimu uliopita ndiyo mambo yalikuwa magumu zaidi walipotolewa katika Hatua ya 16 na Mashujaa FC wakifungwa kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya kufungana bao 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Mara ya mwisho Simba kuingia Faibali ya michuano hiyo ulikuwa msimu wa 2020–21 walipoifunga Yanga 1-0 na kutwaa taji kwa bao pekee la kiungo Mganda, Thadeo Lwanga dakika ya 80 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Aidha, Simba SC inapoteza nafasi ya kuwania Kombe la CRDB ikitoka kukosa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa na RSB Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1 ikifungwa 2-0 Berkane, kabla ya sare ya 1-1 Jumapili iliopita Zanzibar.
Simba SC ambao mwanzoni mwa msimu walifungwa 1-0 na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii – nafasi pekee ya kutwaa taji sasa ni la Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Kuelekea mechi mbili tatu za mwisho, Simba wanazidiwa pointi moja na mabingwa watetezi, Yanga ambao watakutana nao pia Juni 15.