NI NAPOLI MABINGWA WA KABUMBU SERIE A ITALIA, INTER MILAN…
TIMU ya Napoli jana imefanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Italia, Serie A baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cagliari katika mchezo wake wa mwishi wa msimu Uwanja wa Diego Armando Maradona Jijini Napoli.
Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo, kiungo wa Kimataifa wa Scotland, Scott McTominay dakika ya 42 na mshambuliaji wa Kimataifa wa Ubelgiji mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Romelu Lukaku dakika ya 51.
Napoli wanamaliza msimu na pointi 82, moja zaidi ya Inter Milan ambayo jana nayo ilishinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Como mabao ya Stefan de Vrij dakika ya 21 na Joaquin Correa dakika ya 51 Uwanja wa Giuseppe Sinigaglia mjini Como.
Napoli wanatwaa taji la Serie A kwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu na kuzima ndoto za Inter Milan kutwaa taji la pili mfululizo la ubingwa wa Italia.
Kwa matokeo hayo, Inter Milan inaelekeza nguvu zake kwenye Fainali UEFA Champions League dhidi ya Paris St-Germain Jijini Munich, ambako Kocha Simone Inzaghi atajaribu kufuta machungu ya kupoteza Scudetto kwa Napoli.