YANGA YAMTUMIA SALAMU ZA POLE YAO
KLABU ya Yanga imempa pole beki wake Muivory Coast, Kouassi Attohoula Yao na kuombea apone haraka na kurejea kazini.
Yao anasumbuliwa na maumivu ya goti ambayo yamemfanya awe nje ya Uwanja kwa sehemu kubwa ya msimu huu baada ya mwanzo mzuri katika msimu wake wa kwanza akionyesha umuhimu wake kwenye klabu hiyo.
Awali, Yao mwenyewe aliposti picha kwenye ukurasa wake wa Instagram zikiwa zimeambatana na ujumbe; “Let’s normalize the fact that everything should not be so rosy in our lives! Failure really exists the wrong periods and difficulties also have their role in our lives, everyone can go through the hard times, it’s all about time and work in silence to get back to the top.
Anamaanisha kwamba; “Si wakati wote kitu huwa kizuri sana katika maisha yetu! Kufeli hutokea, wakati mbaya na mgumu pia vina nafasi katika maisha yetu. Ni suala la muda tu na kupambana kufanya kazi kimyakimya kurejea kileleni,”.
Kouassi Attohoula Yao aliyezaliwa Desemba 20, mwaka 1996 mjini Anyama nchini Ivory Coast alijiunga na Yanga Julai 14, mwaka 2023 akitokea ASEC Mimosas ya kwao, Abidjan.
Kisoka aliibukia kwenye timu ya vijana ya Mimosas U19, kabla ya kwenda Williamsville O hadi mwaka 2019 akaenda Morocco ambako alichezea klabu za Khouribga na KACM Marrakech, kabla ya kurejea ASEC Mimosas mwaka 2020.
