TIMU ya Simba SC imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC yamefungwa na kiungo Mkongo, Fabrice Luamba Ngoma dakika ya 24, mshambuliaji Mcameroon, Christian Leonel Ateba Mbida dakika ya 30 na winga Mzambia, Joshua Mutale Budo dakika ya 43 baada ya kiungo Mudathir Said Khamis kuanza kuifungia Mbeya City dakika ya 22.
Kwa ushindi huo, Simba itakutana na mshindi kati ya Singida Black Stars na Kagera Sugar zinazotarajiwa kumenyana kesho Uwanja wa CCM LITI mjini Singida.
Nusu Fainali nyingine ya Kombe la CRDB itapigwa kesho baina ya JKT Tanzania na Pamba Jiji Uwanja wa Meja Jenerali Charles Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam - wakati keshokutwa hatua hiyo itakamilishwa kwa mabingwa watetezi, Yanga kumenyana na Stand United Uwanja wa KMC Complex.
Mshindi kati ya JKT Tanzania na Pamba Jiji atakutana na mshindi kati ya Yanga na Stand United katika Nusu Fainali.
0 comments:
Post a Comment