MCHEZO wa kwanza wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Simba SC na Stellenbosch ya Afrika Kusini utapigwa Uwanja wa New Amaan Complex Jumapili ya Aprili 20 kuanzia Saa 10:00 jioni.
Simba SC wamelazimika kuupeleka mchezo huo Zanzibar kufuatia Serikali kufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kwa ukarabati.
Stellenbosch imefika hatua hii baada ya kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek kwa kuwachapa 1-0 Aprili 9, bao la kiungo Sihle Nduli Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo kufuatia kutoka suluhu kwenye mchezo wa kwanza Aprili 2 pia Uwanja wa DHL Cape Town Jijini Cape Town.
Simba SC ilifika Nusu Fainali ya michuano hiyo kwa kuitoa Al Masry ya Misri pia kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya jumla ya 2-2 baada ya kila timu kushinda 2-0 nyumbani.
Al Masry ilianza kushinda 2-0 pia kwenye mchezo wa kwanza Aprili 2 mabao ya washambuliaji Mualgeria, Abderrahim Deghmoum dakika ya 16 na Mnigeria, John Okoye Ebuka dakika ya 89 Uwanja wa New Suez mjini Ismailia.
Simba ikalipa kisasi Aprili 9 kwa mabao ya winga Mkongo, Elie Mpanzu Kibisawala dakika ya 22 na mshambuliaji Mganda, Steven Dese Mukwala dakika ya 32 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Kipa Mguinea wa Simba, Moussa Camara aliokoa mikwaju miwili ya penalti za viungo, Mohamed Gaber Tawfik Hussein ‘Mido Gaber’ na Mahmoud Hamada Awad, huku ya Fakhreddine Ben Youssef pekee ikimpita.
Waliofunga penalti za Simba ni Ahoua, Mukwala, kiungo mshambuliaji Kibu Denis Prosper na beki Shomari Salum Kapombe.
Timu hizo zitarudiana Aprili 27 Uwanja wa DHL Cape Town Jijini Cape Town, Afrika Kusini na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla kati ya RSB Berkane ya Morocco na CS Constantine ya Algeria katika Fainali.
0 comments:
Post a Comment