• HABARI MPYA

        Wednesday, April 09, 2025

        RAIS DK SAMIA AWAMWAGIA PONGEZI WEKUNDU WA MSIMBAZI



        RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameipongeza klabu ya Simba SC kwa kufuzu Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
        Simba SC imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Al Masry ya Misri jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
        Hiyo ilifuatia Simba kushinda 2-0 ndani ya dakika 90, mabao ya winga Mkongo, Elie Mpanzu Kibisawala dakika ya 22 na mshambuliaji Mganda, Steven Dese Mukwala dakika ya 32.
        Ushindi huo ulifanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 kufuatia Al Masry kushinda 2-0 pia kwenye mchezo wa kwanza Aprili 2 mabao ya washambuliaji Mualgeria, Abderrahim Deghmoum dakika ya 16 na Mnigeria, John Okoye Ebuka dakika ya 89 Uwanja wa New Suez mjini Ismailia.
        Kipa Mguinea wa Simba, Moussa Camara ameibuka shujaa kwa kuokoa mikwaju miwili ya penalti za viungo, Mohamed Gaber Tawfik Hussein ‘Mido Gaber’ na Mahmoud Hamada Awad, huku ya Fakhreddine Ben Youssef pekee ikimpita.
        Waliofunga penalti za Simba ni Ahoua, Mukwala, kiungo mshambuliaji Kibu Denis Prosper na beki Shomari Salum Kapombe.
        Simba sasa itakutana na mshindi wa jumla kati ya wenyeji, Zamalek na Stellenbosch ya Afrika Kusini zinazorudiana usiku huu Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo baada ya timu hizo kutoka suluhu kwenye mchezo wa kwanza Aprili 2 pia Uwanja wa DHL Cape Town Jijini Cape Town.
        • Blogger Comments
        • Facebook Comments

        0 comments:

        Item Reviewed: RAIS DK SAMIA AWAMWAGIA PONGEZI WEKUNDU WA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry