Wednesday, April 09, 2025

    NI STELLENBOSCH DARAJA LA SIMBA KWENDA FAINALI CAF


    TIMU ya Simba SC itakutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baadaye mwezi huu.
    Hiyo ni baada ya Stellenbosch kuwatoa mabingwa watetezi, Zamalek kwa kuwachapa 1-0 usiku huu bao la kiungo Sihle Nduli Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo.
    Ni ushindi huo wa ugenini unawakutanisha na Simba kufuatia kutoka suluhu kwenye mchezo wa kwanza Aprili 2 pia Uwanja wa DHL Cape Town Jijini Cape Town.
    Simba SC ilitangulia Nusu Fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa penalti 4-1 kufuatia sare ya jumla ya 2-2 na Al Masry ya kila timu ikishinda 2-0 nyumbani.
    Al Masry ilianza kushinda 2-0 pia kwenye mchezo wa kwanza Aprili 2 mabao ya washambuliaji Mualgeria, Abderrahim Deghmoum dakika ya 16 na Mnigeria, John Okoye Ebuka dakika ya 89 Uwanja wa New Suez mjini Ismailia.
    Na leo Simba imelipa kisasi kwa mabao ya winga Mkongo, Elie Mpanzu Kibisawala dakika ya 22 na mshambuliaji Mganda, Steven Dese Mukwala dakika ya 32 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
    Kipa Mguinea wa Simba, Moussa Camara ameibuka shujaa kwa kuokoa mikwaju miwili ya penalti za viungo, Mohamed Gaber Tawfik Hussein ‘Mido Gaber’ na Mahmoud Hamada Awad, huku ya Fakhreddine Ben Youssef pekee ikimpita.
    Waliofunga penalti za Simba ni Ahoua, Mukwala, kiungo mshambuliaji Kibu Denis Prosper na beki Shomari Salum Kapombe.
    Katika Nusu Fainali, Simba itaanzia nyumbani Aprili 20, kabla ya kwenda kumalizia kazi ugenini Aprili 27 Uwanja wa DHL Cape Town Jijini Cape Town, Afrika Kusini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI STELLENBOSCH DARAJA LA SIMBA KWENDA FAINALI CAF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry