WENYEJI, Namungo FC wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Mabao ya Namungo FC yamefungwa na kiungo Geoffrey Julius Luzendaze dakika ya 15 na beki Mghana, Daniel Amoah dakika ya 67, wakati bao pekee la KMC limefungwa na Kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Somalia, Ibrahim Elias dakika ya 48.
Kwa ushindi huo, Namungo FC inafikisha pointi 27 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tisa, ikiizidi tu wastani wa mabao KMC baada ya wote kucheza mechi 25.
Ligi Kuu inashirikisha timu 16 na mwisho wa msimu mbili zitashuka Daraja na mbili nyingine zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu ya Championship kujaribu tena kubaki Ligi Kuu.
0 comments:
Post a Comment