TIMU za Simba SC na Azam FC zimegawana pointi moja moja baada ya sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Azam FC walitangulia na bao la dakika ya pili tu la winga Mgambia, Gibrill Sillah akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mguinea, Mousa Camara kufuatia krosi nzuri ya Iddi Suleiman ‘Nado’ kutoka kushoto mwa Uwanja.
Simba wakasawazisha dakika ya 25 kwa bao la winga Mkongo, Elly Mpanzu Kibisawala aloyepokea pasi nzuri ya kiungo mshambuliaji Mtanzania, mwenye asili ya Kongo, Kibu Dennis Prosper.
Kipindi cha pili ikawa zamu ya Simba kutangulia kwa bao la beki Abdurazam Mohamed Hamza dakika ya 76 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu wa kiungo Muivory Coast, Jean Charles Ahoua kutoka kulia mwa Uwanja.
Aliyeinusuru Azam kupoteza mchezo wa leo ni winga mzawa chipukizi wa miaka 19, Zidane Sereri kwa kusawazisha bao dakika ya 88 baada ya kupokea pasi ndefu ya kiungo Feisal Salum na kuwatoka mabeki wa Simba kabla ya kumlamba chenga kipa Camara.
Kwa matokeo hayo, Simba inafikisha pointi 51 katika mchezo wa 20, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi nne na mabingwa watetezi, Yanga ambao pia wamecheza mechi moja zaidi.
Kwa upande wao Azam FC wanafikisha pointi 44, nao wanabaki nafasi ya tatu mbele ya Singida Black Stars yenye pointi 38 baada ya wote kucheza mechi 21.
0 comments:
Post a Comment