MABINGWA watetezi, Yanga wamerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya wenyeji, KMC jioni ya leo Uwanj wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Ilikuwa ni siku nzuri kwa kiungo Mburkinabe, Stephane Aziz Ki aliyefunga mabao matatu, mawili kwa penalti dakika ya 18 na 56 na lingine dakika ya 49.
Mabao mengine ya Yanga yamefungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo dakika ya 10, kiungo Mkongo, Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 90’+1 na beki mzawa, Israel Patrick Mwenda dakika ya 90’+4.
Bao pekee la KMC leo limefungwa na kiungo Redemtus Jeremiah Mussa akimtungua kwa shuti la mbali kipa namba moja wa Mali, Djigui Diarra dakika ya 51.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 49 katika mchezo wa 19 na kurejea kileleni, ikiizidi pointi mbili Simba ambayo pia ina mechi moja mkononi.
Kwa upande wao KMC baada ya kichapo cha leo inabaki na pointi zake 22 za mechi 19 nafasi ya saba kwenye ligi ya timu 16.
0 comments:
Post a Comment