BAO la dakika ya 90'+4 la mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo limeinusu Yanga kupoteza mechi ikipata sare ya 1-1 na wenyeji, Tout Puissant Mazembe katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa TP Mazembe Jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
TP Mazembe walitangulia kwa bao la mshambuliaji kinda wa umri wa miaka 20, Cheick Oumar Abdallah Fofana dakika ya 41 akimfunga kipa raia mwenzake wa Mali, Djigui Diarra ambaye hakurejea kipindi cha pili nafasi yake ikichukuliwa Khomeiny Abubakar.
Kwa matokeo hayo, Mazembe wanafikisha pointi mbili wakibaki nafasi ya tatu kwenye kundi hilo, wakati Yanga inayookota pointi ya kwanza leo inaendelea kushika mkia baada ya mechi tatu za awali - wote wakiwa nyuma ya Al Hilal Omdurman ya Sudan yenye pointi sita na MC Alger ya Algeria yenye pointi nne.
Al Hilal Omdurman watakuwa wageni wa MC Alger kukamilisha mechi zao tatu za mzunguko wa kwanza kuanzia Saa 4:00 usiku wa leo Uwanja wa Julai 5 1962 Jijini Algiers.
0 comments:
Post a Comment