WENYEJI, CS Constantine wametoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Mohamed-Hamlaoui mjini Constantine, Algeria.
Beki na Nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alianza kuifungia Simba dakika ya 24 kwa shuti la mbali kutoka upande wa kushoto wa Uwanja bao ambalo lilidumu hadi mapumziko.
Dakika moja baada ya kuanza kipindi cha pili beki Abdulrazack Mohamed Hamza alijifunga akijaribu kuokoa shambulizi la kona na kuipatia CS Constantine bao la kusawazisha, kabla ya mshambuliaji Brahim Dib kuwafungia wenyeji bao la ushindi dakika ya 50.
Kwa ushindi huo, CS Constantine wanafikisha pointi sita na kuendelea kuongoza Kundi A, wakati Simba wanabaki na pointi zao tatu sawa na Bravos do Maquis ya Angola ambao leo wameifunga CS Sfaxien ya Tunisia 3-2 Uwanja wa Novembro 11 mjini Luanda.
CS Sfaxien baada ya kupoteza mechi zote mbili za kwanza pamoja na ile waliyofungwa 1-0 na CS Constantine wiki iliyopita Jijini Tunis wanashika mkia Kundi A.
0 comments:
Post a Comment