WENYEJI, Tabora United wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mabao yote ya Tabora United leo yamefungwa na mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Ma Olongi Makambo moja kila kipindi akimc hambua kipa namba moja wa timu ya taifa ya Sudan kwa kichwa dakika ya 37 na 68.
Kwa upande wao, Azam FC bao lao pekee lilifungwa na beki wa Kimataifa wa Mali, Yoro Mamadou Diaby dakika ya 71 kwa kichwa akimtungua kipa Hussein Salum Masalanga 'Buffon'.
Kwa ushindi huo, Tabora United wanafikisha pointi 24 katika mchezo wa 14, ingawa wanabaki nafasi ya tano wakizidiwa pointi tatu na Singida Black Stars ambao pia wana mechi moja mkononi.
Pamoja na kupoteza mchezo wa leo, Azam FC wanaendeleza kuongoza Ligi Kuu wakibaki na pointi zao 30 kufuatia kucheza mechi 14, mbele ya Simba SC yenye pointi 28 na mabingwa watetezi, wenye pointi 27 baada ya wote kucheza mechi 11.
0 comments:
Post a Comment