MABINGWA watetezi, Yanga hatimaye wamezinduka baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na mshambuliaji wa Kimataifa wa Zambia, Kennedy Musonda dakika ya 50 na kiungo Muivory Coast, Peodoh Pacôme Zouzoua dakika ya 67.
Huo unakuwa ushindi wa kwanza baada ya timu hiyo kupoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu 1-0 mbele ya Azam FC, 3-1 kwa Tabora United zote za Ligi Kuu na 2-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika Ligi ya Mabingwa Afrika zote nyumbami, Dar es Salaam.
Ni ushindi wa kwanza kwa kocha mpya, Mjerumani Sead Ramovic baada ya kurithi mikoba ya Muargentina, Miguel Angel Gamondi aliyefukuzwa kufuatia vipigo mfululizo vya Azam na Tabora United.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 27 na kusogea nafasi ya pili, ikizidiwa pointi moja na watani wa jadi, Simba SC baada ya wote kucheza mechi 11, wakati Namungo FC inabaki na pointi zake tisa za mechi 12 sasa nafasi ya 14.
0 comments:
Post a Comment