KIUNGO wa Manchester City, Rodrigo Hernández Cascante 'Rodri' ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka duniani, Ballon d'Or akiwaangusha nyota watatu wa Real Madrid alioingia nao Fainali, Mbrazil Vinicius Junior, Mspaniola mwenzake, Dani Carvajal na Muingereza, Jude Bellingham.
Katika sherehe za utoaji wa tuzo hiyo ukumbi wa Théâtre du Châtelet Jijini Paris usiku wa jana, Nyota wa Barcelona, Aitana Bonmatí Conca ameshinda Tuzo hiyo upande upande wa wanawake kwa mwaka wa pili mfululizo.
Tuzo ya Mwanasoka Bora chipukizi, ijulikanayo kama Kopa Trophy imekwenda kwa kinda wa Barcelona, Mspaniola Lamine Yamal, wakati Mfaransa Kylian Mbappé wa Real Madrid na Muingereza, Harry Kane wa Bayern Munich wameshinda tuzo ya Ufungaji Bora ijulikanayo kama Gerd Muller Trophy.
Tuzo ya Kipa Bora ijulikanayo kama Yashin Trophy imekwenda kwa mlinda mlango wa Aston Villa, Muargentina Emiliano Martínez, wakati mwanamama Mspaniola Jennifer Hermoso Fuentes anayechezea klabu ya Liga MX ameshinda Tuzo ya Socrates, ambayo hutolewa kwa mwanasoka anayefanya shughuli za kibinadam na kijamii.
Real Madrid imeshinda Tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka kwa Wanaume, wakati FC Barcelona imebeba Tuzo kwa Wanawake, Kocha Bora Wanawake ni Emma Hayes na Kocha Bora wa WanaumeCarlo Ancelotti.
Rodi anakuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu ya England kushinda Ballon d'Or tangu Mreno Cristiano Ronaldo mwaka 2008.
Rodri aliyewasili ukumbi wa Théâtre du Châtelet akitembea kwa gongo huku akisaidiwa baada ya kuumia Septemba mwaka kwenye mchezo dhidi ya Arsenal - alikuwa na msimu bora zaiid maishani mwake 2023-24 baada ya kushinda taji la nne mfululizo la Ligi Kuu ya England na kuisaidia Hispania kushinda Euro 2024.
0 comments:
Post a Comment