MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya watani, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Iliwalazimu kusubiri hadi dakika ya 86 mabingwa hao mara tatu mfululizo kushangilia ushindi wao kwa bao la kujifunga la beki Kelvin Sospeter Kijiri aliyekuwa anajribu mpira uliopigwa na kiungo na Mkongo, Maxi Mpia Nzengejli.
Mpira uliozaa bao hiloi ulianzia kwenye shuti la mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama ambao ulipanguliwa na Mguinea, Moussa Camara na kumkuta Nzengeli aliyeunganisha langoni ukagonga nguzo na wakati unarudi uwanjani Kijiri akaujaza nyavuni akijaribu kuokoa.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 15 katika mchezo wa tano na kusogea nafasi ya pili ikizidiwa pointi moja Singida Black Stars ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.
Kwa upande wao Simba baada ya kipigo cha leo ambacho ni cha nne mfululizo kutoka kwa watani tangu uliopita inabaki na pointi zake 13 baada ya kucheza mechi sita.
0 comments:
Post a Comment