WENYEJI, FC Inter Milan usiku wa jana wamelazimishwa sare ya kufungana mabao 4-4 na katika mchezo wa Serie A baina ya mahasimu hao wakubwa zaidi Italia uliofanyika Uwanja wa Giuseppe Meazza Jijini Milan.
Katika mchezo huo mtamu wa ‘funga nikufunge’ mabao ya Inter Milan yalifungwa na viungo Mpoland, Piotr Zieliński mawili yote kwa penalti dakika ya 15 na 37, Muarmenia Henrikh Mkhitaryan dakika ya 35 na beki Mholanzi, Denzel Dumfries dakika ya 53.
Juventus waliotoka nyuma kwa mabao 4-2, mabao yalifungwa na mshambuliaji Mserbia, Dušan Vlahović dakika ya 20, kiungo Mmarekani, Timothy Weah dakika ya 26 na mshambuliaji kinda wa miaka 19 Mturuki aliyezaliwa Ujerumani, Kenan Yıldız mawili dakika ya 71 na 82.
Yıldız aliiokoa Juventus kwa mabao yake hayo baada ya kuinuliwa na Kocha Thiago Motta kutoka benchi dakika ya 62 kwenda kuchukua nafasi ya Timothy Weah, mtoto wa Mwanasoka Bora wa Dunia wa zamanı, George Weah.
Kwa matokeo hayo Inter Milan inafikisha pointi 18 na inabaki nafasi ya pili ikiendelea kuizidi pointi moja Juventus na wote wakiwa nyuma ya Napoli yenye pointi 22 baada ya hizo zote kucheza mechi tisa.
0 comments:
Post a Comment