RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samiah Suluhu Hassan amezipongeza klabu za Simba na Yanga kwa kufuzu hatua ya makundi michuano ya Afrika.
Rais Samia ameandika usiku huu kwenye akaunti yake ya Instagram; “Hongera kwa Klabu ya Yanga na Klabu ya Simba kwa kuibuka washindi katika michezo yenu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ya mwishoni mwa juma. Yanga mkifanya vizuri katika Klabu Bingwa na Simba katika Kombe la Shirikisho. Endeleeni kutupa burudani. Hamasa yangu na dua za kheri toka kwa mamilioni ya Watanzania daima ziko pamoja nanyi,”.
Yanga walifuzu Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika inayochezwa kwa mtindo wa makundi baada ya ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya timu ya Benki ya Biashara Ethiopia, CBE SA (Commercial Bank of Ethiopia Sports Association) usiku wa jana Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katika mchezo wa marudiano Hatua ya 32 Bora, mabao ya Yanga yalifungwa na Mzambia, Clatous Chama dakika ya 35, mzawa Clement Mzize dakika ya 46, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 74 na 90’+3, mzawa Mudathir Yahya dakika ya 88 na Mkenya, Duke Abuya dakika ya 90.
Kwa matokeo hayo, Yanga inafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa 7-0 kufuatia kuichapa CBE SA 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita bao la Mzimbabwe, Prince Dube dakika ya 45’+1 Uwanja wa Abebe Bikila Jijini Addis Ababa.
Kwa upande wa Simba wametinga 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya katika mchezo wa marudiano Hatua ya 32 Bora jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Simba, kwani walilazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa na Ahli kwa bao la mshambuliaji wa Kimataifa wa Angola, Agostinho Cristovao Paciencia ‘Mabululu’ dakika ya 17.
Mshambuliaji mzawa, Kibu Dennis Prosper alianza kuifungia Simba bao zuri la kusawazisha kwa tik-tak dakika ya 36, kabla ya mshambuliaji Mcameroon, Christian Leonel Ateba Mbida kufunga bao la pili dakika ya 45’+1 na winga mzawa Edwin Charles Balua akafunga la tatu dakika ya 90.
Kwa matokeo hayo, Simba inakwenda hatua ya 16 Bora ambayo huchezwa kwa makundi kufuatia sare ya bila mabao kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Jijini Tripoli.
0 comments:
Post a Comment