MLEZI wa klabu ya Singida Black Stars Mwigulu Lameck Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameiomba klabu ya Yanga imruhusu kiungo Yusuph Ally Kagoma (28) aichezee Simba.
Yanga imeweka pingamizi usajili wa Kagoma kutoka Singida Black Stars kwenda Simba, kwa sababu mchezaji huyo alisaini mkataba wao awali, lakini akaenda kusaini na kwa wapinzani pia.
Waziri Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi, mkoani Singida kwa tiketi ya chama tawala, CCM amesema kwamba anafahamu undani wa suala la Yusuf Kagoma, lakini anaisihi Yanga imhurumie na kumruhusu acheze Simba ili kuokoa kipaji chake.
"Nimewaomba viongozi wa Yanga wasamehe yote, waondoe shauri dhidi ya Kagoma, wamuache awe huru akaitumikie Simba kwa maslahi mapana ya mpira wa Tanzania na kwa faida ya mchezaji mwenyewe," amesema Waziri Nchemba kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Katika kufafanua sakata hilo, Waziri Nchemba amesema; "Ni kweli Kagoma alisaini mkataba Yanga, na baadae akasaini Simba, Najua kutokwenda kwake Yanga na badala yake kusaini Simba hata sio Masuala ya Fedha. Tutatumia muda sana tukitaka kuchimba haya. Kagoma ni mtoto wetu,".
Waziri Nchemba amesema Yanga ni klabu kubwa ambayo ina mambo mengi muhimu ya kuyatilia mkazo ili kuyafanikisha kuliko kutumia nguvu hizo kuzuia Kagoma aisicheze, ingawa ni kweli amesaini klabu zote mbili.
"Yanga ni klabu kubwa sana na ina mambo muhimu ya kuyawekea nguvu kuyafanikisha kuliko kuweka nguvu Kagoma aisicheze licha ya ukweli kwamba alistahili achezee Yanga,"amesema.
0 comments:
Post a Comment