WANARIADHA wa kiume wa Tanzania Alphonce Felix Simbu na Gabriel Gerald Geay wametoka mikono mitupu katika mbio ndefu kwenye Michezo ya Olimpiki leo Jijini Paris, ambazo Mhabeshi Tamirat Tola ameshinda Medali ya Dhahabu.
Angalau Simbu alimaliza nafasi ya 17 akitumia muda wa 2:10:03, lakini Geay alikuwa nje ya kinyang'anyiro kabisa akimaliza nafasi ya 74 kati ya wakimbiaji 81.
Tola amevunja rekodi ya Olimpiki kwenye Marathoni iliyowekwa kwenye Michezo ya mwaka 2008 Jijini Beijing nchini China na Sisay Lemma, ambaye hakushiriki michezo ya mwaka huu kutokana na kuwa majeruhi na nafasi yake akapewa Tamirat wiki mbili za mwisho.
"Sisay aliniambia ilikuwa vizuri kwake kujitoa na mimi kwenda kushindana. Alisema, 'Unaweza kufanya vizuri zaidi yangu kutokana na hali yangu.' Ni shukrani kwake, ushindi huu ni wa kwake pia kwa kunipa fursa hii," amesema Tola.
Wanariadha wengine wa Tanzania, Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri watakimbia kesho kwenye Marathoni ya Wanawake katika kilele cha Michezo ya Olimpiki iliyoanza Julai 26.
Simbu na Geay wanaungana na wanamichezo wenginewatatu wa Tanzania waliotolewa awali, ambao ni waogeleaji Collins Phillip Saliboko na Sophia Anisa Latiff pamoja na Mcheza Judo, Andrew Thomas Mlugu.
Tola mwenye umri wa miaka 32 alitumia muda wa 2:06:26, akifuatiwa na Mbelgiji Bashir Abdi mzaliwa wa Somalia aliyeshinda Medali ya Fedha akitumia muda wa 2:06:47, wakati Benson Kipruto wa Kenya ameshinda Medali ya Shaba akitumia 2:07:00.
0 comments:
Post a Comment