KIKOSI cha Simba Queens kimeondoka Dar es Salaam mchana wa leo kwenda Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA inayotarajiwa kuanza Jumamosi wiki hii, Agosti 17 hadi Septemba 4.
Chini ya Kocha Juma Mgunda na Msaidizi wake, Mussa Mgosi – Wachezaji walioondoka ni makipa; Janeth Shija, Carolyne Rufa na Gelwa Yonah, mabeki ni; Fatma Issa ‘Densa’, Dotto Evarist, Ruth Ingosi, Violeth Nicholaus, Emiliana Isaya, Wincate Kaari, Esther Mayalla na Daniela Ngoyi.
Viungo ni Elizabeth Wambui, Josephine Julius, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Precious Christopher, Amina Bilal, Ritticia Mabbosa, Jackline Albert, Viviian Corazone, Mary Saiki na Asha Djafar, wakati washambuliaji ni Shelder Boniface, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Jentirx Shikangwa.
Simba Queens imepangwa Kundi B pamoja na PVP Buyenzi ya Burundi, FAD ya Djibouti na Kawempe Muslim ha Uganda na mechi zake zitapigwa Uwanja wa Abebe Bikila, wakati Kundi B ambalo mechi zake zitapigwa Uwanja wa Addis Ababa – linaundwa na wenyeji, CBE, Police Bullets ya Kenya, Sports Department ya Rwanda na Yei Joint Stars ya Sudan Kusini.
Simba Queens, itaanza kuwania taji hilo Jumapili wiki hii, Agosti 18 dhidi ya FAD, kabla ya kumenyana na Kawempe Muslim Agosti 20 na kumalizia na PVP Agosti 22.
Hiyo itakuwa michuano ya nne ya CECAFA kutafuta timu ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mwaka 2021 nchini Kenya ambako wenyeji, Vihiga Queens waliibuka mabingwa, mwaka 2022 Jijini Dar es Salaam wenyeji, Simba Queens wakibeba taji na mwaka jana nchini Uganda, JKT Queens ya Tanzania ikitwaa Umalkia wa kandanda Afrika Mashariki na Kati.
0 comments:
Post a Comment