KOCHA wa Yanga SC, Muargentina Miguel Angel Gamondi amesema kwamba Simba imebadilika kila kitu, hivyo mchezo wa leo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii baina ya watani hao wa jadi utakuwa mgumu.
Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari jana Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam ambako mchezo huo utafanyika kuanzia Saa 1:00 usiku wa leo, Gamondi amesema huu ni msimu mpya hata wapinzani wake pia wamebadilika kila kitu.
Pamoja na hayo, Gamondi amesema timu yake ipo imara kiakili na kimwili na wamejianda vya kutosha kwa ajili ya mchezo huo kuwakabili washindi hao wa Ngao ya Jamii msimu uliopita.
"Hakuna tunachohofia, sijapata wasaa mzuri wa kuwatazama wapinzani, kwani mechi zake nyingi hazikuonyeshwa, lakini hiyo si changamoto kubwa, kwani naanda timu yangu kwa asilimia 75, asilimia 25 ndiyo natumia kumchunguza mpinzani,” amesema Gamondi na kuongeza;
"Hakuna siri kwenye mpira kila kitu lazima kiwe hadharani, kesho (leo) ni siku muhimu sana, kwani ni mechi ya mtoano, hatupaswi kufanya makosa, tunapaswa kuwa makini kwenye kila idara ili kupata matokeo mazuri, naamini mashabiki wetu watajitokeza kwa wingi kwa lengo la kutupa hamasa,”.
Gamondi amesema anawaheshimu sana wapinzani wote anaokutana nao, hususan mechi hiyo ya wapinzani wakubwa wa nchi' "Mchezo wa derby hakuna kibonde kwenye mchezo huo, kwani ni mchezo maalumu sana, najua mpinzani wetu ana timu mpya, wachezaji wapya, wote kwa pamoja watachukua fursa hii kuonesha ubora wao," amesema.
Kwa upande wake mwakilishi wa wachezaji, kipa mpya Khomein Abubakar amesema kwamba wamejandaa vizuri kuwakabili Simba wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri.
"Tumejiandaa vizuri sana na tuko tayari, wachezaji wana ari na wote tunawahakikishia kuwa wachezaji tunakwenda kupambana, naamini kesho tutafanya vizuri,” amesema mlindamlango huyo aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars.
0 comments:
Post a Comment