KOCHA Muargentina wa Yanga, Miguel Angel Gamondi amesema kwamba watakuwa na mchezo mgumu wa Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC kesho kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Benjmin Mkapa Jijini Dar es Salaam lakini watajitahidi washinde.
Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Gamondi amesema kwamba siku zote mechi dhidi ya Azam FC huwa ngumu.
"Napenda kucheza aina hii ya mechi, tumecheza na Simba sasa Azam ni kipimo sahihi kuelekea msimu mpya, tumekuwa na mwendelezo mzuri tokea tumecheza fainali Zanzibar, napocheza na wapinzani wagumu basi unaimarisha zaidi kikosi chako kiushindani, nina matumaini kesho tutacheza vizuri,” amesema Gamondi na kuongeza.
“Tumetumia jitihada kubwa kwenye mchezo uliopita, sina wasiwasi na kikosi changu kwani nina kikosi kipana ambacho kinanipa uhuru wa kupanga wachezaji tofauti, nina jua kesho tutakuwa na mchezo mgumu sana lakini nina imani na vijana wangu,".
“Huu ni mchezo wa fainali, unapaswa kuwa makini sana, nakumbuka vyema mchezo uliopita pale Zanzibar, tayari tunayo picha sahihi tunapaswa kwenda na mbinu gani dhidi ya Azam Fc, niwahakikishie Yanga Sc ni timu imara sana, ukitazama mchezo uliopita Simba walitengeneza nafasi moja tu kwa sababu tulikuwa imara kwenye kila idara," amesema.
Gamondi amesema watacheza mechi hiyo kama ambavyo wamekuwa wakicheza mara kwa mara na kwamba jambo muhimu ni kuhakikisha hawafanyi makosa madogo madogo wala kuruhusu bao, huku akijivunia vijana wake kucheza kitimu zaidi.
“Mchezo uliopita Zanzibar Azam walicheza kwa kujihami sana na kwa tahadhari kubwa mno, tulitengeneza nafasi nyingi sana na hatukucheza tofauti na tunavyochezaga, mchezo ujao ni tofauti na ule kwani hivi sasa Yanga tuna vipaji vikubwa sana ambavyo tunaweza kubadilisha matokeo yaliyopita,"ameema Gamondi.
Yanga imeingia Fainali baada ya kuwachapa watani, Simba SC 1-0 juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, wakati Azam FC iliitoa Coastal Union kwa kuichapa mabao 5-2 juzi pia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo utatanguliwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu baina ya Coastal Union na Simba SC kuanzia Saa 10:00 jioni.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Juni 2, mwaka huu katika Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la CRDB na Yanga ikaibuka na ushindi wa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila mabao ndani ya dakika 120 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Msimu uliopita kwenye Ngao ya Jamii timu hizo zilikutana katika Nusu Fainali Agosti 9, mwaka jana na Yanga ikaichapa Azam FC 2-0, mabao ya Stephane Aziz Ki dakika ya 85 na Clement John Mzize dakika ya 89 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Hata hivyo, ni Simba iliyotwaa taji hilo kwa kuifunga kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga Agosti 13, mwaka jana.
Mechi mbili za Ligi Kuu msimu uliopita kila timu ilishinda moja, Oktoba 23, mwaka jana Stephane Aziz Ki alifunga mabao yote ya Yanga ikishinda 3-2 Uwanja Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam - huku mabao ya Azam yakifungwa Gibrill Sillah na Prince Dube Mpumelelo aliyehamia Jangwani.
Machi 17 mabao ya Gibrill Sillah dakika ya 19 na Feisal Salum Abdallah dakika ya 51 yaliipa Azam FC ushindi wa 2-1 dhidi ya Yanga ambayo ilitangulia kwa bao la Clement Francis Mzize dakika ya 10.
0 comments:
Post a Comment