TIMU ya Azam Football Club mapema leo asubuhi imetambulisha jezi zake za msimu mpya kwenye boti ya Kilimanjaro Eight ‘The Falcon Sea’ wakati wa safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.
Ni jezi aina tatu zenye mvuto, uimara na ubora wa hali ya juu – ya kwanza ni ya nyumbani, ambayo ni ya rangi nyeupe na dhahabu, ya pili ni ya ugenini yenye rangi ya buluu na dhahabu, na ya tatu ni nyeusi na dhahabu, ambayo inatambulika hivyo hivyo, kama jezi ya tatu, maarufu Third Kit.
Baadaye Saa 9 Alasiri Azm FC wakafanya uzinduzi rasmi wa jezi hizo kwenye jengo la Michenzani Mall, Unguja, visiwani Zanzibar ambako mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi, Tabia Maulid Mwita.
Wakati huo huo: Kikosi cha Azam FC kimerejea leo asubuhi Jijini Dar es Salaam kutoka Morocco ambako kilikuwa kimeweka kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya.
Azam FC wamekwenda moja kwa moja kambini kwao, Azam Complex, Chamazi kuendelea na maandalizi ya msimu ambao watauanza kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union ya Tanga Agosti 8 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Ikiwa nchini Morocco, Azam FC ilicheza mechi tatu za kujipima nguvu, Julai 20 ikishinda 3-0 dhidi ya Union Yacoub El Mansour, Julai 27 ikitoa sare ya 1-1 na Union de Touarga, kabla ya kuchapwa 4-1 na Wydad Athletic FC Julai 29.
Azam FC ambayo msimu ujao pamoja na mashindano ya nyumbani pia itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika – itakuwa na safari ya Rwanda pia kucheza na wenyeji, Rayon Sports katika mchezo mwingine wa kirafiki.
0 comments:
Post a Comment