KLABU ya Simba imemtambulisha kiungo Omary Abdallah Omary (23) kutoka Mashujaa FC ya Kigoma kuwa mchezaji wake mpya wa tisa kuelekea msimu ujao.
Huyo anakuwa mchezaji mpya wa tisa Simba SC baada ya mabeki wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
Wengine ni kiungo wa ulinzi, Mnigeria, Augustine Okejepha (20) kutoka Rivers United ya kwao, Port Harcourt na winga Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe na kiungo mshambuliaji, Débora Fernandes Mavambo (24) mwenye uraia pacha wa Kongo - Brazzaville na Angola kutoka Mutondo Stars ya Zambia.
Wapya wengine ni washambuliaji Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
Aidha, Simba SC jana ilimtambulisha Kocha Mkuu mpya, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wake mpya Mkuu, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchika aliyeondoka April 28, mwaka huu.
Fadlu Davids amekuja na safu yake nzima ya Wasaisizi, wote raia wenzake wa Afrika Kusini, Kocha Msaidizi, Darian Wilken, Kocha wa Makipa, Wayne Sandilands, Kocha wa Fitness, Riedoh Berdien na Mchambuzi, Mueez Kajee.
Kikosi kinatarajiwa kuondoka Jumatatu kwenda mjini Ismailia nchini Misri kuweka kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya.
0 comments:
Post a Comment