TIMU za England na Uholanzi zimefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya 'Euro 2024' baada ya kuzitoa Uswisi na Uturuki usiku wa jana nchini Ujerumani.
Ilianza England kuitupa nje Uswisi kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Dusseldorf Arena Jijini Dusseldorf.
Mshambuliaji mwenye asili ya Cameroon, Breel Donald Embolo anayechezea Monaco ya Ufaransa alianza kuifungia Uswisi dakika ya 75, kabla ya mshambuliaji mwenye asili ya Nigeria, Bukayo Ayoyinka Temidayo Saka kuisawazishia England dakika ya 80.
Ukawadia wakati mzuri kwa kipa wa Everton, Jordan Lee Pickford aliyeokoa mkwaju wa penalti wa beki wa Manchester City, Manuel Obafemi Akanji na kuipeleka England Nusu Fainali ya Euro 2024 ambako sasa itakutana na Uholanzi.
Waliofunga penalti za England ni Cole Palmer, Jude Bellingham, Bukayo Saka, Ivan Toney na Trent Alexander-Arnold, wakati waliofunga penalti za Uswisi ni Fabian Schar, Xherdan Shaqiri na Mohamed Zeki Amdouni.
Nao Uholanzi wakaimaliza Uturuki ndani ya dakika 90 kwa kuichapa 2-1 Uwanja wa Olympia Jijini Berlin.
Mabao ya Uholanzi yalifungwa na mabeki, Stefan de Vrij wa Inter Milan ya Italia dakika ya 70 na Mert Muldur wa Fenerbahce aliyejifunga dakika ya 76 kufuatia beki mwingine, Samet Akaydin wa Fenerbahce kuanza kuifungia Uturuki dakika ya 35.
Nusu Fainali ya kwanza itapigwa Jumanne kati ya Hispania na Ufaransa, wakati ya pili itafuatia Jumatano baina ya Uholanzi na England, mechi zote zikianza Saa 4:00 usiku.
0 comments:
Post a Comment