KOCHA mpya wa Simba SC, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini jana alitumia muda fulani kumpa maelekezo mshambuliaji mpya, Mganda Steven Mukwala aliyesajiliwa kutoka Asante Kotoko ya Ghana.
Simba SC imeweka kambi mjini Ismailia nchini Misri kujiandaa na msimu mpya ambao watauanza kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wa jadi, Yanga Agosti 8 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Simba SC imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota wapya 14, ambao ni mabeki, Kelvin Sospeter Kijiri (24) kutoka Singida Big Stars, Mburkinabe Valentin Nouma (24) kutoka FC Saint-Éloi Lupopo ya (DRC), wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
Wengine ni viungo, Awesu Ally Awesu (27) kutoka KMC, Mnigeria, Augustine Okejepha (20) kutoka Rivers United ya kwao, Port Harcourt, Omary Abdallah Omary (23) kutoka Mashujaa FC ya Kigoma, Yusuph Ally Kagoma (28) kutoka Singida Big Stars, Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe, Débora Fernandes Mavambo (24) mwenye uraia pacha wa Kongo - Brazzaville na Angola kutoka Mutondo Stars ya Zambia.
Kuna washambuliaji pia, Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
Fadlu Davids amekuja na safu yake nzima ya Wasaisizi, wote raia wenzake wa Afrika Kusini, Kocha Msaidizi, Darian Wilken, Kocha wa Makipa, Wayne Sandilands, Kocha wa Fitness, Riedoh Berdien na Mchambuzi, Mueez Kajee.
0 comments:
Post a Comment