MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC leo wameanza vibaya michuano ya kuwania Kombe la Mpumalanga International baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Augsburg ya Ujerumani Uwanja wa Mbombela, Mpumalanga nchini Afrika Kusini.
Mabao ya Augsburg waliomaliza nafasi ya 11 kwenye Ligi ya Ujerumani, Bundesliga msimu uliopita yamefungwa na beki wa kushoto Mdenmark, Mads Pedersen dakika ya 37 na mchezaji mpya, winga wa kushoto Mjapan, Masaya Okugawa dakika ya 80.
Bao pekee la Yanga limefungwa na mshambuliaji mpya, Jean Othos Baleke dakika ya 86 akimalizia krosi ya Mkomgo mwenzake, kiungo Maxi Mpia Nzengeli kutoka upande wa kushoto.
Yanga SC waliowasili Afrika Kusini Alhamisi kuweka kambi ya kujiandaa na msimu - watateremka tena dimbani Jumatano kumenyana na wenyeji, TS Galaxy, kabla ya kukamilisha mechi zake za kujipima kwa kucheza na Kaizer Chiefs Jumapili, Julai 28 Uwanja wa Toyota mjini Bloemfontein.
0 comments:
Post a Comment