TIMU ya Azam FC jana imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Union de Touarga katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa mazoezi mjini Ben Slimane nchini Morocco.
Bao la Azam FC limefungwa na mchezaji mpya, mshambuliaji Nassor Saadun Hamoud aliyesajiliwa kutoka Geita Gold na huo unakuwa mchezo wa pili ya kirafiki katika kambi yao ya kujiandaa na msimu mpya nchini Morocco baada ya Julai 20 kushinda 3-0 dhidi ya wenyeji wengine, Union Yacoub El Mansour.
Azam FC ambayo msimu ujao pamoja na mashindano ya nyumbani pia itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika - itakamilisha mechi zake za kirafiki kwenye kambi hiyo Jumatatu kwa kucheza na wenyeji wengine, Wydad Athletic, kabla ya kikosi kurejea nchini mapema Agosti.
Azam FC watakuwa na safari ya Rwanda kucheza na Rayon Sports, kabla ya kurejea tena nchini tayari kwa mchezo wake wa kwanza wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union Agosti 8 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment