TIMU ya Azam FC imechapwa mabao 4-1 na wenyeji, Wydad Athletic FC katika mchezo wa kirafiki uliofanyika usiku wa jana Uwanja wa El Bacchir mjini Mohammedia nchini Morocco.
Mabao ya Wydad yamefungwa na washambuliaji Mohamed Rayhi, Mounir El Habach, Chouaib Fardi na Mohamed El Ouardi, wakati bao pekee la Azam FC limefungwa na beki Msenegal, Cheikh Sidibé kwa penalti.
Huo unakuwa mchezo wa tatu wa kirafiki katika kambi yao ya kujiandaa na msimu mpya nchini Morocco baada ya Julai 20 kushinda 3-0 dhidi ya wenyeji wengine, Union Yacoub El Mansour na Julai 27 kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Union de Touarga.
Azam FC ambayo msimu ujao pamoja na mashindano ya nyumbani pia itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika - sasa itarejea nchini mapema Agosti na kuunganisha safari kwenda Rwanda kucheza na wenyeji, Rayon Sports katika mchezo mwingine wa kirafiki.
Azam FC inatarajiwa kuuanza msimu mpya kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union Agosti 8 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment