TIMU ya Al Hilal FC ya Sudan jana imeibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Red Arrows FC ya Zambia katika mchezo wa Kundi B Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Uwanja wa Azam Comlpex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Al Hilal yalifungwa na Adama Coulibaly matatu, dakika za tisa, 55 na 63 na mengine mawili, Mohamed Abdelathman Yousif dakika ya 14 na 24.
Kwa ushindi huo, Al Hilal inafikisha pointi sita kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya ASAS ya Djibouti katika mchezo wa kwanza, wakati Red Arrows FC inabaki na pointi zake tatu ilizovuna kwenye ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Mechi nyingine ya Kundi B jana Gor Mahia iliambulia sare ya 1-1 na ASAS hapo hapo Uwanja wa Azam Comlpex.
Levin Joseph Odhiambo alianza kuifungia Gor Mahia dakika ya 39, kabla ya Warsama Houssein Said kuisawazishia ASAS dakika ya 41.
Baada ya mechi za kwanza, Al Hilal inaongoza Kundi B kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Red Arrows tatu, Gor Mahia moja sawa na ASAS.
Timu itakayoongoza Kundi ndiyo itafuzu Nusu Fainali ikiongozana na mshindi wa pili Bora wa makundi yote.
0 comments:
Post a Comment