• HABARI MPYA

    Sunday, June 09, 2024

    BEKI ALIYEIPA TUKUYU STARS UBINGWA WA LIGI KUU 1986, MATHEW AFARIKI DUNIA

    BEKI wa zamani wa Kimataifa wa Tanzania, Suleiman Mathew Luwongo (pichani) amefariki dunia mapema leo katika hospitali ya Amana, Ilala Jijini Dar es Salaam Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
    Mathew aliyezaliwa Agosti 18, mwaka 1965 aliibukia Kil Tex ya Arusha mwaka 1984 hadi mwaka 1985 akaenda Tukuyu Stars na kuipandisha Ligi Daraja la Kwanza, sasa Ligi Kuu mwaka 1986 na msimu huo huo akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
    Mwaka 1988 alisajiliwa Yanga SC na mwaka 1989, kabla ya kuhamia kwa watani, Simba SC mwaka 1989 alikocheza hadi mwaka 1990 akajiunga na Ndovu ya Arusha ambayo aliichezea hadi mwaka 1994 akahamia Milambo ya Tabora. 
    Suleiman Mathew (wa tatu kushoto waliochuchumaa) akiwa na kikosi cha Yanga 1988
    Suleiman Mathew (wa tatu kutoka kushoto waliosimama) akiwa na kikosi cha Simba SC mwaka 1989

    Mwaka 1995 alikwenda kujiunga na Small Simba ya Zanzibar hadi 1996 alipojiunga tena na Ndovu, wakati imekwishabadilishwa jina na kuwa AFC ya Arusha kufuatia kutemwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
    Alicheza AFC Arusha hadi mwaka 1997 akaamua kustaafu soka na kuwa kocha akafundisha timu mbalimbali zikiwemo Mto Singida, baadaye Singida United 2000. 
    Baadaye akaamua kuachana kabisa na soka na kujikita kwenye Siasa na amekuwa Diwani wa Kata ya Vijibweni, kabla ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
    Msiba upo nyumbani kwake, Kigamboni, Vijibweni Jijini Dar es Salaam na mazishi yatafanyika kesho baada ya sala ya Alasiri makaburi ya Vijibweni. 
    Inna lilah wainna ilayh rajiuun. Mungu ampumzishe kwa amani Suleiman Mathew.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BEKI ALIYEIPA TUKUYU STARS UBINGWA WA LIGI KUU 1986, MATHEW AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top