KLABU ya Azam FC imeendelea kujiimarisha kuelekea msimu ujao wa michuano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kusajili mchezaji mpya wa tano na wa kwanza mzawa, ambaye ni mshambuliaji Adam Omary Adam (27) kutoka Mashujaa ya Kigoma.
Adam ni kama anarejea nyumbani, kwani kisoka aliibukia katika akademi ya klabu hiyo mwaka 2011 chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul hadi mwaka 2014 alipokwenda kutafuta uzoefu wa kucheza Ligi Kuu.
Alicheza timu mbalimbali kwanza kwa mkopo, kabla ya kuhamishwa rasmi akianzia Mbao FC ya Mwanza, Tanzania Prisons, JKT Tanzania, Al-Wahda Tripoli ya Libya, Polisi Tanzania, Ihefu SC na Mashujaa.
“Tunathibitisha kuwa tumeingia naye mkataba wa mwaka mmoja, tayari kabisa kuitumikia Azam FC msimu ujao 2023/24,”imesema taarifa ya Azam FC kuhusu Adam mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita amefunga mabao saba katika Ligi Kuu.
Akiwa Akademi ya Azam FC, kati ya 2011 na 2014, Adam alizisaidia timu za vijana za U17 na U29 kubeba mataji yakiwemo Kombe la Uhai na michuano ya Rollingstone ya Arusha.
Adam anakuwa mchezaji mpya wa tano Azam FC kuelekea msimu ujao baada ya beki wa kati, Yoro Mamadou Diaby kutoka Stade Malien alipokuwa anacheza kwa mkopo kutoka akademi ya Yeleen Olympique ya Mali na kiungo mshambuliaji, Muivory Coast, Franck Tiesse kutoka Stade Malien.
Wengine ni Wacolombia, kiungo Ever Meza kutoka Leonnes ya kwao na mshambuliaji Jhonier Blanco kutoka Aguilas Doradas ya kwao pia, Colombia.
0 comments:
Post a Comment